Kikosi cha Azam FC kimewasili salama jijini Mbeya tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City FC.
Mchezo wa miamba hiyo ya Tanzania Bara umepangwa kupigwa kesho Jumanne (Septemba 13) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, kuanzia saa kumi jioni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye kurasa za Mitandao ya Kijamii za klabu ya Azam FC, imethibitisha kuwasili salama kwa kikosi cha klabu hiyo jijini Mbeya.
“#LandingMbeya Tumefika salama jijini Mbeya, tayari kabisa kwa mchezo wetu dhidi ya Mbeya City.” imeeleza taarifa ya Azam FC
Kwa mara ya kwanza Azam FC kesho Jumanne (Septemba 13) itaongozwa na Kocha Mkuu mpya kutoka Ufaransa Denis Lavagne, akichukuwa nafasi ya Abdihamid Moallin.
Hadi sasa Azam FC imefikisha alama tano katika msimamo wa Ligi Kuu (Ikishinda mchezo mmoja dhidi ya Kagera Sugar, ikitoka sare dhidi ya Geita Gold FC na Young Africans).
Kwa upande wa Mbeya City imeshajikusanyia alama nne katika msimamo wa Ligi Kuu (Ikishinda dhidi ya Dodoma Jiji FC, ikipoteza dhidi ya Singida Big Stars na kuambulia sare dhidi ya Tanzania Prisons).
0 Comments