Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent
Bashungwa amepiga marufuku Halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kuvuka na
fedha mwaka mwingine wa fedha (Bakaa) na kuzielekeza kwenye matumizi yasiyofaa.
Bashungwa ameyasema hayo leo Septemba 24, 2022 alipokuwa akikagua ujenzi wa
shule ya Sekondari ya Lalaji iliyopo katika Kata ya Lalaji, Halmashauri ya
Wilaya ya Hanang', mkoani Manyara.
Amesema kuwa kumeibuka tabia ya Halmashauri kuvuka na fedha mwaka mwingine wa
fedha na kuzielekeza kwenye matumizi yasiyofaa ikiwamo safari zisizo kuwa na
tija badala ya kuzielekeza kwenye utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.
Amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafanya tathmini ya fedha zote
za bakaa ili ziende kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo na sio matumizi
mwingine yasiyofaa.
"Hizi fedha za bakaa zipelekwe kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo kama
ujenzi wa madarasa, mabweni, mabwalo, vituo vya afya, na ujenzi wa miundombinu
ya barabara ili kuwasaidiaa wananchi,"amesema.
Ameongeza kuwa Wananchi wanakiu ya kupata maendeleo hawatafurahi kuona
tunazunguka nchi nzima kwa kutumia bakaa ya fedha ambayo ilitakiwa kutekeleza
miradi ya maendeleo.
Amemuagiza Kaimu Katibu Mkuu Dkt.Charles Msonde kuhakikisha anafanya uchambuzi
wa fedha za bakaa zilizobaki katika halmashauri na kutoa taarifa ya matumizi ya
fedha zilizobaki kama bakaa na matumizi yake.
0 Comments