BILIONI 160 KUJENGA VYUMBA VYA MADARASA 8,000
Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia utoaji kiasi cha sh bilioni 160 kwa ajili ya
ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 vitakavyoweza kupokea wanafunzi wa ziada wa
kidato cha kwanza 400,000 ambao ni zao la Elimumsingi bila ada.
Hayo yamesemwa leo Septemba 28, 2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa
wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato
cha kwanza januari, 2023
Amesema fedha hizo tayari zimeshaingia kwenye akaunti za shule za sekondari
2,439 zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya
kidato cha kwanza 2023.
Amesema kwa sasa fedha hizo zimeshatumwa na kupokelewa kwenye halmashauri zote
184, kulingana na upungufu uliowasilishwa na kila Halmashauri husika.
Idadi ya wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022
ilikuwa ni 907,802 ikilinganishwa na wanafunzi 422,403 waliohitimu kidato cha
nne, hivyo kuhitaji kuongezeka miundombinu ya madarasa na vyoo yenye
kutosheleza wanafunzi 485,399 wa ziada.
Ili kutatua changamoto hiyo, Serikali ya awamu ya sita ilitoa kiasi cha sh.
Bilioni 240 zilizofanikisha ujenzi wa madarasa 12,000, shule shikizi 3,000 na
mabweni 60.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, idadi ya wanafunzi walioandikishwa
darasa la kwanza ilikuwa kubwa sana, kwa kulinganisha na miaka iliyotangulia.
Kwa mukatadha huo wanafunzi waliopo darasa la saba mwaka 2022, ndio zao la
kwanza la matokeo ya Elimumsingi bila ada,”amesema Bashungwa.
Ameeleza kuwa katika hali ya kawaida matarajio ni kuwa nafasi zilizopo kwa
ajili ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza, zitokane na uwepo wa shule
mpya za sekondari, ujenzi wa miundombinu mipya na nafasi zilizoachwa na
wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne.
0 Comments