KAMPUNI ya Japan Tobacco Incorporation (JTI) imeahidi kununua kilo milioni 30
za tumbaku kutoka kwa wakulima wa Tanzania katika msimu ujao wa kilimo.
Ahadi hiyo imetolewa leo (Jumatatu, Septemba 26, 2022) na Rais na Mtendaji Mkuu
wa JTI, Bw. Masamichi Terabatake mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
aliyetembelea ofisi zao ili kuwahakikishia utekelezaji wa mazungumzo
yaliyofanyika wakati wa mkutano wa TICAD 8, jijini Tunis, Agosti, mwaka huu.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu amesema uamuzi wa kampuni hiyo
kuongeza kiwango cha ununuzi wa tumbaku utatoa ahueni kwa wakulima wa Tanzania
ambao walikuwa hawana uhakika wa soko la zao hilo.
“Leo Bodi ya Wakurugenzi imetangaza uamuzi wa kununua kilo milioni 30 za
tumbaku kutoka kilo milioni 14 ambazo walinunua msimu uliopita. Hii ni fursa
kubwa kwa wakulima wetu kwani kiasi hicho ni zaidi ya uzalishaji wa zao la
tumbaku Tanzania,” amesema.
“Miaka ya nyuma makampuni yaliyokuwa yakinunua tumbaku yalizoea kuwapangia
wakulima wetu idadi ya kilo za kununua, kwa hiyo hata uzalishaji haukuwa mkubwa
sana. Nikiwa ziarani Tabora, nilikutana na viongozi wakuu wa vyama vya wakulima
wa zao hili, na waliomba kupewa fursa ya kuongeza soko, kwa hiyo wakulima sasa
waongeze uzalishaji ili tufikie lengo hili,” amesisitiza.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya JTI, Bw. Mutsuo Iwai na
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Bw. Takashi Araki.
Waziri Mkuu yuko Japan akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya
Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Bw. Shinzo Abe yanayotarajia kufanyika kesho.
0 Comments