Kamishna Jenerali wa mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 15,2022 Jijini Dar es Salaam.
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata watu 9 akiwemo kocha wa makipa wa timu ya Simba Club Muharami Sultan (40) wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilo 34.89 pamoja na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa ya kulevya aina ya bangi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Gerald Kusaya alisema mbali na mtuhumiwa Sultan ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji wa zamani wa timu ya Simba Club, wengine waliokamatwa ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sports Academy kilichopo Tuangoma Kigamboni, Kambi Seif (40).
Alisema watuhumiwa wengine ni Seleman Matola (24) mkulima na mtoto wa dada yake na mtuhumiwa Seif, Said Matwiko (41) fundi seremala, Maulid Mzungu (54) ambaye anaundugu wa mtuhumiwa Sultan ambaye ni kocha wa Simba.
“Wengine waliokamatwa ni John Andrew (40) mkazi wa Magore Kitunda, huyu ni mfanyabiashara pia ana jukumu la kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka kituo cha Cambiasso Sports Academy, Rajabu Dhahabu (32) mfanyabiashara na mkazi wa Tabata Segerea, Hussein Pazi (41) pamoja na Ramadhan Chalamila (27)” alisema Kusaya.
Kusaya alisema katika tukio jingine mamlaka hiyo ilimkamata mtuhumiwa Abdulnasir Kombo (30) ambaye ni mkazi wa Kaloleni jijini Arusha akiwa na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa ya kulevya aina ya bangi kama moja ya malighafi aliyokuwa akiiuza katika eneo la jiji hilo.
Imewezesha na
@dceatanzania
0 Comments