MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
imesema kutokana na udhibiti kuwa mkubwa wanaoendelea kuufanya katika biashara
ya dawa za kulevya, wafanyabiashara wa dawa hizo wameendelea kubuni mbinu mpya
za usafirishaji wa dawa za kulevya ili kukwepa kukamatwa ikiwemo ya raia wa
kigeni kuwatumia wanawake wa kitanzania kufanya biashara hiyo.
Akizungumza leo Juni 19,2023 mbele ya waandishi wa habari
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya
Aretas Lyimo amesema baada ya kubaini mbinu hizo wamechukua hatua za
kuzidhibiti huku akitoa onyo kwa wanawake ambao wanatumiwa na raia wa kigeni
kufanyabiashara ya dawa za kulevya.
“Mbinu mojawapo inayotumika ni raia wa kigeni kuanzisha
mahusiano ya kimapenzi na wanawake wa kitanzania zaidi ya mmoja na kuficha dawa
za kulevya kwenye makazi ya wanawake hao huku wao wakipanga nyumba tofauti na
wanakoishi wapenzi wao.
“Hali hii husababisha wanawake wa kitanzania kuingia kwenye
matatizo makubwa ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria huku wanaume
wakiwakana wanawake hao. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,
imejipanga kikamilifu kupambana na biashara ya dawa za kulevya,”amesema
Kamishina Jenerali Lyimo.
Aidha amesema wote wanaojihusisha au wenye mpango wa
kujihusisha na biashara hiyo, waache mara moja au wajisalimishe wenyewe kabla
hawajafikiwa na mkono wa sheria.Pia, wananchi wanapaswa kuwa makini na mizigo
wanayopewa kubeba au kuhifadhi pasipo kujua ndani yake kuna nini.
“Wanawake wanatakiwa kuwa makini zaidi kwani katika baadhi
ya matukio, wamekuwa wakitumiwa na wapenzi wao hasa raia wa kigeni kusafirisha
na kupokea mizigo wasiyoijua na wakati mwingine mizigo hiyo huwa na dawa za
kulevya na hivyo hujikuta matatani.
“Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa
za Kulevya kinaeleza kwamba, ni kosa kusafirisha dawa za kulevya, na mtu yoyote
akithibitika kutenda kosa hilo atawajibishwa kisheria ikiwa ni pamoja na
kifungo kisichopungua miaka 30 au kifungo cha maisha gerezani,”amesema.
Aidha amesema Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha
inamaliza tatizo la dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii.Kutokana na kuwepo
madhara makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia yanayotokana na matumizi
ya dawa za kulevya.
Ameongeza ni vema wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa
Serikali kwa kuwafichua wote wanaojihusisha na matumizi na biashara ya dawa za
kulevya ili kwa pamoja tuweze kulikomboa taifa kutoka katika janga hilo na
katika kuhakikisha biashara na matumizi ya dawa za kulevya
yanatokomea nchini, Mamlaka imejikita katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la
dawa za kulevya kwa jamii.
Amesema lengo ni kupanua wigo wa utoaji elimu huku
akifafanua Mamlaka imeingia makubaliano na TAKUKURU kutumia klabu zao
zilizokwisha anzishwa kwenye shule na vyuo kutoa elimu juu ya tatizo la dawa za
kulevya. Hivyo, elimu ya kupambana na rushwa na dawa za kulevya itatolewa
kupitia klabu hizo.
0 Comments