Serikali Kuweka Misingi Imara Kuwainua Wanawake Kiuchumi - Waziri Gwajima.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima.

Serikali Nchini, imedhamiria kuwainua Wanawake kiuchumi kwa kuweka msingi unaochochea mabadiliko yanayojielekeza katika ukuaji wa uchumi.


Kauli hiyo, imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini yaliyofanyika Kijiji cha Olevolosi, Kata ya Kimnyak, Wilaya ya Arumeru, Arusha.

Amesema, nia ya Rais Dkt. Samia ni kuwainua Wanawake huku akitaja baadhi ya mambo yanayotekelezwa na kuwagusa Wanawake kwa kurejea takwimu, ikiwemo mikopo ya Sh. bilioni 713.8 iliyotolewa Julai 2022 hadi Machi, 2023.

“Mikopo hii, ilizalisha ajira 3,122,104 kwa Wanawake ikiwa ni asilimia 52 na mikopo hiyo pia ilienda kwa wajasiriamali 2,203,838 Wanawake wakiwa ni asilimia56,” alisema Waziri Gwajima.

Kuhusu Mwanamke na ardhi, amesema idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi imekuwa ikiongezeka ukilinganisha na awali, kwani kufikia 2021/22 jumla ya Hatimiliki za Kimila 1,171,884 zimetolewa na Wwanawake waliopata ni 406,915.

Aidha, kwenye eneo la biashara ya mazao ya Kilimo, Dkt.Gwajima amewaasa Wanawake kufanya biashara kwa kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya Kilimo na kuhakikisha bidhaa zina alama ya msimbomilia (Barcode), vifungashio nadhifu na vyenye ubora ili kukidhi vigezo kwenye masoko makubwa ya ndani na nje.


Post a Comment

0 Comments