"Kuna Wakimbizi Wamepata Teuzi Za Uongozi Tanzania" CDF Jenerali Jacob John Mkunda.


Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa maoni kwamba kuendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa Wakimbizi na Waomba hifadhi Nchini Tanzania ni tishio la kiusalama kwani taarifa zilizopo ni kwamba wapo Wakimbizi na Waomba hifadhi ambao wameajiriwa Serikalini na wengine wamepewa teuzi Serikalini katika nafasi zenye maamuzi.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Jacob John Mkunda amesema hayo mbele ya Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu leo January 22,2024 wakati wa Mkutano wa Saba wa CDF na Makamanda Jijini Dar es salaam.

CDF amesema “Changamoto kubwa katika Mikoa yetu ya magharibi kwa sasa ni uwepo wa Wakimbizi na Waomba hifadhi wa muda mrefu, Tanzania imekuwa ikipokea maombi ya Wakimbizi na Waomba hifadhi kutoka Burundi tangu mwaka 1972, Rwanda tangu mwaka 1994 na DRC tangu mwaka 1996, idadi ya Wakimbizi 27000 kutoka Burundi wa mwaka 1972 hawakuwekwa katika kambi za Wakimbizi badala yake Serikali iliamua kuwagawanya katika Vijiji 73 vilivyopo Mkoa wa Kigoma”

“Wakimbizi hawa na Familia zao bado wanaendelea kuishi katika Vijiji hivyo na kwa kutumia mbinu mbalimbali uhakikisha uzao wao unapata Uraia wa Tanzania bila kufuata Sheria, Serikali ya Tanzania na Burundi zimekuwa zikiwashawishi Wakimbizi hao kurejea Nchini mwao bila mafanikio

“Mh. Rais kuanzia January 01,2023 hadi December 31,2023 jumla ya Waomba hifadhi 138,149 walipokelewa Tanzania ambao sehemu kubwa ni kutoka DRC, Rwanda na Burundi, kutokana na mahojiano ya awali imebainika kuwa Waomba hifadhi wengi wamekuja Tanzania kwa sababu za kiuchumi kwani Tanzania imebainika kuwa na fursa nyingi za kiuchumi kuliko Nchi walizotoka, hata hivyo sababu hizo zinazowafanya Wakimbie Nchi zao zinawakosesha sifa sa kupewa hadhi ya ukimbizi”

“Ni maoni yetu kwamba kuendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa Waomba hifadhi na Wakimbizi hawa Nchini ni tishio la kiusalama kwani taarifa zilizopo ni kwamba baadhi ya Waomba hifadhi hao au Wakimbizi au Familia zao wameajiriwa Serikalini kwa nafasi mbalimbali na wengine wamepewa teuzi Serikalini katika nafasi zenye maamuzi”

Post a Comment

0 Comments