DIT Yatoa Mafunzo ya Kutengeneza Magari Yanayotumia Umeme Kwa Mafundi Gereji.


Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), imetoa mafunzo kwa mafundi gereji yanayohusu kutengeneza magari na vyombo vingine vya moto vinavyotumia umeme.

Mafunzo hayo ya siku tano yamehudhuriwa na mafundi 31 kutoka Halmashauri tano za jiji la Dar es Salaam yakilenga kutoa ujuzi wa namna ya kufanya matengenezo kwenye magari ya umeme ikiwa ni teknolojia ambayo inakuja kwa kasi nchini.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyotolewa na DIT, Dkt. Essebi Nyari amesema,
"DIT ni taasisi ya elimu ya kwanza nchini Tanzania ambayo imeanza na imeweza kutoa mafunzo haya ya matengenezo ya magari yanayotumia umeme na si hivyo tu Taasisi kupitia Kampuni yake Tanzu imeweza kufanya miradi mbali mbali inayotumia nishati salama kama baiskeli na bajaji za umeme pamoja na kuongeza mfumo wa gesi asilia kwenye magari" amesema Dkt.Nyari.


Dkt, Nyari amekazia kuwa matumizi ya nishati salama ni mfumo unaokuja kwa kasi ambao utapelekea kuwa na uhitaji mkubwa wa mafundi wa magari ya umeme hivyo DIT kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaanza kuandaa mazingira ambayo yataifanya jamii kuwa na mafundi wabobezi.

Nae Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo Prof.Ezekiel Amri akitoa vyeti kwa wahitimu amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na walimu wa DIT ya kutoa mafunzo ambayo amesema kuwa yatasaidia kuongeza idadi kubwa ya mafundi hasa kutakapokuwa na ongezeko kubwa la vyombo vya moto vinavyotumia umeme.

Aidha, ameahidi kuwa DIT ipo tayari kuhakikisha kuwa matatizo yaliyopo kwenye jamii yanapata ufumbuzi yakinifu kwa kutumia wataalam waliopo pamoja na Teknolojia.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wakiwakilishwa na fundi Eliud kutoka kampuni ya Nduvuni auto Garage ameishukuru Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa kutoa mafunzo ambayo anaamini yatakuwa chachu kwa vijana na kusaidia kuzalisha ajira za kutosha nchini.
"Kwa niaba ya wenzangu napenda kuishukuru DIT kwa kuleta mafunzo haya kwa kweli yatatusaidia kufanya kazi kwa kujiamini lakini ukiwa na ujuzi unaweza kujiajiri hivyo niombe mafunzo haya yawe endelevu ili tunufaike zaidi." amesema Eliud.


Post a Comment

0 Comments