Tanzania Kuondolewa Kundi la Nchi Maskini Sana Duniani.


Utekelezaji wa Dira ya 2025 umekuwa na mafanikio ya kuridhisha ikiwa ni pamoja na kulifikisha taifa kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati cha chini ( low-middle income countries) mwaka 2020, Aidha mwaka huu wa 2024 Umoja wa Mataifa umeanza mchakato wa kuiondoa nchi yetu katika kundi la nchi masikini sana duniani ( least developed countries). Kwa upande wa viashiria mahususi vya maendeleo, hali ya umasikini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 36 mwaka 2000 hadi asilimia 26. 4 mwaka 2018. Umasikini wa chakula umepungua kutoka asilimia 19 mwaka 2000 hadi asilimia 8 mwaka 2018, vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa kila vizazi hai 1000 vimepungua kutoka 147 mwaka 1996 hadi 43 mwaka 2022. 

Upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya afya umeongezeka kutoka 64% mwaka 2015 hadi takribani 80% mwaka 2022. Uandikishaji wa watoto katika shule za msingi umeongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 1999 hadi asilimia 97 mwaka 2022, kiwango cha ufaulu katika shule za msingi kimeongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2000 hadi asilimia 80 mwaka 2020 na upatikanaji wa maji safi na salama vijijini umeongezeka kutoka asilimia 50 hadi asilimia 79.6 mwaka 2023”

“ Licha ya mafanikio hayo niliyoyataja kwa kifupi na mengine yataelezwa baadaye, taifa letu bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali. Aidha viwango vya mafanikio yetu bado ni vya chini vikilinganishwa na nchi za Kusini Mashariki mwa Asia ambazo tulikuwa karibu sawa katika miaka ya 1960. Kiwango cha mahitaji ya msingi cha asilimia 26. 4 ambayo maana yake ni watu milioni 16.3 bado ni cha juu sana na hakikubaliki lakini kadhalika kiwango cha udumavu cha asilimia 30 katika taifa lenye ziada ya chakula hakiridhishi ikiwa tunalenga kukuza nguvu kazi imara” Dkt. Mpango.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza katika Kongamano la Kwanza la Kitaifa Kuhusu Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 linalofanyika katika ukumbi wa Nkurumah Hall, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jumamosi Juni 08, 2024.

Post a Comment

0 Comments